Sekondari ya Abbey

 
SEKONDARI yetu ya Wavulana (Abbey Secondary School) ilipokea wanafunzi wake wa kwanza hapo Januari 7, 2007. Ni shule ya kulala inayomilikiwa na kuongozwa na Watawa wa Abasia. Kundi la kwanza la wanafunzi kuanza masomo lilikuwa na wanafunzi takriban 42. Kundi hili lilimaliza kidato cha nne mwaka 2010 kwa mafanikio makubwa. Pamoja na upya wa shule, kundi la kwanza liliifanya shule yetu kushika nfafasi ya kwanza katika shule za Ukanda wa Kusini. Kati ya shule zaidi ya  2000 katika nchi nzima, shule ilishika nafasi ya nane.  
   Mwanzo mgumu - wahenga walisema. Kuanza mradi huu wa shule haikuwa kitu rahisi hata kidogo. Baada ya majadiliano na tafakari nyingi kati ya miaka 2004-2006, jumuiya ilikata shauri kuanzisha shule hii. Wajibu wa kutekeleza mradi huu uliwekwa mikononi mwa Padre Augustino Ombay OSB aliyeiongoza shule katika miaka minne ya kwanza. Kwa jitihada nyingi aliweza kuipatia shule kundi la waalimu hodari ambao kwa ushirikiano wao waliweza kuweka msingi bora kabisa wa shule hii. Matokeo ya mazuri ya mwaka 2010 ni ushahidi wa kutosha wa bidii na umahiri wa waalimu na wafanyakazi wa shule hii. Kutokana na ubora wa shule, idadi ya wanafunzi inaendelea kukua kila mwaka. Ni lengo na nia ya Jumuiya yetu kuipanua shule zaidi na zaidi ila kutoa elimu bora kwa vijana wengi zaidi.

 
  Sekondari yetu ni zaidi ya shule. Sisi kama wamisionari tunaamini kuwa, ili mwanadamu akue na kutambua sehemu na mchango wake katika jamii, anahitaji zaidi ya elimu ya vitabuni au ya darasani. Kwa sababu hiyo, shule hii ni pia kituo cha malezi – malezi si tu ya kiakili bali ya kiroho, kimaadili, kijamii na kiutu kwa ujumla. Kuwa na sekondari kwetu ni utekelezaji wa sera ya kichungaji katika kubadilisha maisha ya watu na kuwapa matumaini kwa siku za mbele. Kwa sababu hiyo Watawa wetu wanashirikana bega kwa bega pamoja na waalimu na wafanyakazi katika kutekeleza utume huu.  
  Kiujumla shule yetu inaongozwa kwa kufuata maadili ya Kikristu. Hii haimaanishi kuwa wasio Wakristu au Wakatoliki hawana nafasi shuleni. Hata kidogo. Uhuru wa dini wa kuabudu unazingatiwa kwa heshima zote. Vijana wanafunzi wanahimizwa daima, si tu kuzielewa vyema imani zao, bali pia kuwa wazi na tayari kuzielewa na kuheshimu imani za wengine. Kwa sababu hiyo, wanafunzi wetu ingawa wanatokea katika mazingira tofauti kabisa ya kidini, wanaishi, kusoma, kucheza na kufanya kazi pamoja bila migongano.   
 

Licha ya masomo ya kawaida, wanafunzi wa shule yetu wanahimizwa kushiriki katika shughuli zingine zozote ziwezazo kukuza ufahamu wao. Hivyo msisitizo unatolewa katika kujifunza elimu ya kompyuta, michezo, kazi za mikono, kukuza imani yao na pia kukuza ufahamu wao katika mambo ya kijamii. Elimu siyo tu ufunguo wa maisha ila pia nguvu imwezeshayo mwanajamii kujijengea maisha bora kwa siku za usoni. Na hili ndilo lango la shule yetu: kuifanya iwe mahali ambapo taifa la kesho linaweza kujitayarisha kwa changamoto za maisha katika ulimwengu wetu unaobadilika kila kukicha.

<< Rudi Mwanzoni    **   Wasiliana na Shule>> ** Washirika Wetu >>