Sala na Liturjia

 

Maisha ya kiroho ya Wabenediktini yamejengwa na  mihimili miwili: " Sala na kazi." Maisha yetu ya Jamii nzima ya Ndanda yanafuata mihimili hiyo miwili. Kwa kawaida sisi huamka mapema asubuhi na kusali sala au masifu ya asubuhi na kisha kuadhimisha Ekaristi takatifu kabla ya kuanza kazi zetu za mikono za kila siku. Tofauti na mashirika mengine ya kitawa ambao wana utamaduni wa kusali sala zao kwa kusoma, sisi, kama Wabenediktini wengine duniani kote, tunaimba sala zetu kwa kutumia tuni za Kigregoriani (Gregorian Chant).

 
 
  Miaka ya 1980 vijana wa Kitanzania walianza kujiunga na jumuiya ya Ndanda. Hivyo jumuiya ya mseto kati ya wamisionari kutoka Ulaya na ndugu wa kizalendo ilizaliwa. Hapo iliamuliwa kutumia lugha ya Kiswahili katika sala na ibada za pamoja. Sr Barbara Ruckert OSB kutoka Tutzing alikuwa msaada mkubwa na wa pekee katika kutimiza adhima hiyo. Mwaka 1994 tulichapisha nakala ndogo Antifonale, ijulikanayo kwa jina la "Masifu ya Jioni." Kilikuwa tu kijitabu kidogo chenye masifu ya jioni ya juma nzima. Hatua kwa hatua tulianza kuimba, kwanza siku moja katika juma, tukaendelea siku mbili katika juma na hatimaye kila siku. Vitabu vingine viliongezwa, kwa ajili ya Majilio, Noeli, Kwaresima na Pasaka.  
 

 Hatimaye mwaka 2000 tulipata"Antifonale yetu ya Kiswahili“. Sr. Barbara alitayarisha kitabu hiki, akishirikiana na Sr Elisabeth Kerp OSB kutoka Peramiho. Tulianza kutumia kitabu hiki mwanzoni mwa mwaka 2001. Wakati kitabu hiki cha kwanza kikitumika, vitabu vilivyoongezwa kwa ajili ya vipindi vya  Majilio, Noeli, Kwaresma na Pasaka. Melodia hizi tuzitumiazo zimekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Ikumbukwe pia kuwa Ndanda si tu utawa ila parokia pia. Kwa hiyo licha ya "Sala za Vipindi" za Watawa, ibada ya Misa inaadhimishwa kila siku - Watawa na Waumini kwa pamoja.

 

<<Mwanzoni