Sakharani & Kurasini

  SAKHARANI: Shamba la Sakharani lililoko kwenye milima ya Usambara liko kama kilometa 150 hivi kutoka bandari ya Tanga. Mwaka 1946, jumuiya ya Ndanda ilinunua sehemu kubwa ya ardhi kutoka kwa Mwingereza mmoja. Ardhi hii ilikuwa itumike kwa malengo ya kilimo. Uwanda huu wenye meta 1300 kutoka usawa wa bahari, unaifanya Sakharani kuwa sehemu nzuri kwa kupanda miche mbalimbali kama miti ya kwinini, makadamia, kahawa, migomba, zabibu, viazi na aina nyingi za mboga. Kutokana na shughuli zote hizi, watu wengi wa mazingira ya jirani wamenufaika kwa kupata ajira.
 

Idadi ya wanajumuiya inabadilika kati ya watatu hadi watano kutegemea shughuli zinazofanyika na upatikanaji wa ndugu kutoka nyumba mama ya Ndanda. Licha ya kazi za shamba, wanajishughulisha na kazi za kichungaji kwanye parokia za Sakharani, Soni na maeneo yanayozizunguka. Ipo pia karakana ndogo ya kukarabati magari, useremala na pia ufugaji wa ng’ombe, kuku na nguruwe. Sakharani yatumika pia kama nyumba ya mapumziko kwa wageni. Wengi wa vijana wanaojiunga na utawa wa Ndanda wanafanya matayarisho yao Sakharani.

Email: benedictinefatherssakharani@gmail.com

  KURASINI: Prokura ya Mt. Maurus Dar es Salaam (inajulikana pia kama Kurasini A, sambamba na Barabara ya Kilwa) ni moja kati ya mali za kwanza kabisa za Wabenediktini hapa Tanzania. Kurasini ilikuwa ya kwanza kufanywa makao ya Msimamizi wa Kitume wa misioni ya Zanzibar Kusini – kama eneo hilo lilivyojulikana enzi hizo. Mwaka 1978, serikali iliamua kukarabati na kupanua bandari ya Dar es Salaam ambapo mali na eneo la prokura ilimegwa katika mradi huo. Kwa hiyo prokura ikalazimika kusogezwa nyuma kilometa moja hivi, ii kutoa nafasi kwa upanuzi wa bandari.  
 

Leo Kurasini inatoa huduma kama prokura ya kusafirishia vifurushi vinavyohitajika na kutumika kwa shughuli za kimisonari. Kwa kawaida ndugu wawili wanaishi na kufanya kazi huko Kurasini. Licha ya shughuli za kiprokura, wanajishughulisha na upokeaji na utunzaji wa wageni ambao hawakomi kupita Kurasini. Kadiri nafasi inavyoruhusu ndugu zetu husaidia kazi za kichungaji kwenye parokia jirani na kutoa huduma za kiroho katika nyumba za masista.

Email: bfkur.dsm@dar.bol.co.tz

Tel +255 222 11 3449

<<Mwanzoni