Uchapishaji - Ndanda Mission Press

 KIWANDA CHA UCHAPISHAJI Ndanda (NMP – Ndanda Mission Press) ambacho kilisajiliwa mwaka 1935 kina idara mbili: Uchapishaji (Printing) na Uhariri (Publishing). Lengo la awali la NMP ilikuwa kuchapisha vitabu vya teolojia, ikiwa ni pamoja na Biblia, liturjia, vitabu vya kichungaji, vitabu vya ibada na vya masomo ya kiroho. Lengo la pili lilikuwa kuchapisha vitabu vinavyohusu matibabu, mambo ya kijamii na historia. Baadaye ulifuata uchapishaji wa vitabu vya watoto, hasa hadithi asilia za Kiafrika, na vya burudani kama vile riwaya. 
  Uchapishaji wa vitabu vya Katekesi ulikuwa ni muhimu sana kwa ajili ya elimu ya dini katika shule za msingi katika Tanzania nzima. Pd. Alkuin Bundschuh OSB alianzisha mfumo wa kuwa na vitabu kwa ajili ya mafundisho ya Katekesi katika shule za msingi. Baadaye aliungwa mkono na Pd. Leo Van Kessel CSSp na kufanya kazi pamoja na kuhariri vitabu saba kwa ajili ya walimu na wanafunzi. Kati ya vitabu muhimu vya katekesi vilivyochapwa na NMP ni mfululizo wa “Watoto wa Mungu,” ambavyo pia kutafsiriwa kwa lugha za Kiteso na Kikalenjini (Kenya).  
   Mfululizo mwingine ulijulikana kama “Wananchi Kuchambua Teolojia,” ambavyo vilikuwa msaada mkubwa kwa mapadre katika kuhuburi Injili. Utafsiri wa Agano Jipya na Zaburi ulifanyika chini ya uongozi wa P. Alkuin ukifuatiwa na uchapishaji wa mfululizo mwingine uliojulikana kama “Tufikirie ...” chini ya Pd. Sebald Hofbeck. Katika uwanja wa Liturjia vitabu muhimu vilichapishwa kama tafsiri ya Kanuni ya Misa (kabla ya Mtaguso), Chuo cha Sala na baadaye Nyimbo za Liturjia (I &II) chini ya Pd. Thomas Eriyo.

 
 

Katika nyanja ya mambo ya kijamii vitabu mbalimbali vilichapishwa kama: Msichana, je? Mvulana je?, Uzazi wa Mpango (BOM), Haki na Amani, Maandishi ya Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa, Uongozi na Saikolojia. Katika eneo la kihistoria NMP huchapisha vitabu mbalimbali juu ya makabila ya Tanzania. Katika milenia mpya NMP inajishughulisha zaidi kuchapisha vitabu vya dini na ya kiliturjia kwa ajili ya ya madhehebu mbalimbali ya Kikiristu. Hata hivyo kutokana na kupanuka kwa mahitaji, NMP inatayarisha na kuchapa vitabu vya aina zote, kadi, fomu zihitajikazo maofisini, madaftari ya watoto wa shule, kalenda, n.k.

 

<<Rudi Mwanzoni * Wasiliana na NMP >>